SIGN IN TO CHAT

WELCOME TO ALLAMANO SEMINARY - MOROGORO

TO PROCLAIM THE GOSPEL TO ALL NATIONS

Saturday, November 3, 2012


MISA YA KUMUOMBEA MKUU WA SHIRIKA LA WAMISIONARI WA CONSOLATA TANZANIA PADRE SALUTARIS LELLO MASAWE ALIYEFARIKI KWA AJALI YA MAJI HUKO BAGAMOYO TAREHE 25 OKTOBA, 2012.
Padre Saltaris Masawe alikuwa Padre wa Shirika la Consoalata mzaliwa wa hapa Tanzania, alipata daraja la Upadre mwaka 1993, jimboni Moshi mkoani Kilimanjaro. Na amefanya kazi katika nchi mbalimbali ambako wamissionari wa Consolata wanafanya kazi. Amewahi kufanya kazi nchini Ethiopia, Italia na baadae  shirika lilimtuma hapa Tanzania ili arudi kuwaimarisha ndugu zake. Mara kwa mara Padre Lello alipenda kusema hivyo kwamba amerudi kuwahudumia ndugu zake watanzania.
Tarehe 25 Oktoba, 2012 Padre Salutaris akiwa na wakuu wa shirika kutoka nchi nyingine za Afrika alikwenda Bagamoya pamoja na mambo mengine walienda kuogelea kama sehemu ya mapumziko yao, na hapo ndipo mauti yalimkuta akiwa anaogelea Baharini, mwili wake ulionekana siku iliyofuata yaani tarehe 26 Oktoba.
Hapa kwetu katika nyumba ya malezi ya Mwenye Heri Padre Yosefu Allamano Morogoro, jioni ya tarehe 26 tulifanya Misa jioni saa kumi na mbili kwaajili ya kumuombea Baba yetu Massawe na  misa hiyo iliongozwa na Padre Hipolith Marandu IMC ambae pia ni mlezi na mwalimu wa Tauhidi (Teolojia) hapa seminarini. Katika Misa hiyo padre Marandu alimuelezea marehemu alivyo mfahamu tangu alipokuwa nae Kenya akiwa shule, baadaye nchini Italia na sasa akiwa hapa Tanzania. Alisema alikuwa ni padre aliyeuishi upadre wake na alilihudumia shirika na kanisa kwa moyo wote, alililetea shirika heshima kila alipotumwa kufanya kazi na yeye mwenyewe aliheshimika ndani ya Tanzania na nje ya Tanzania. Alikuwa kweli mmissionari mwafrika ambae hakujificha kuonesha uafrika wake popote alipokuwa. Aliporudi hapa nyumabani alipewa kazi ya Gazeti la Enendeni, kazi ambayo aliifanya kwa weledi mkubwa na hata kuliinua gazeti kuwa na hadhi sana hapa Tanzania. Mwaka jana mapadre wa shirika la Consolata hapa Tanzania waliona ni vema wamkabidhi madaraka ya kuliongoza shirika, nae kwa moyo mkuu aliipokea hiyo kazi na akawa Padre mwafrika mconsolata wa kwanza kuwa mkuu wa shirika hapa Tanzania. Padre Marandu alitualika kusali kwaajili ya shirika hapa Tanzania na ulimwenguni kote, lakini pia kwaajili ya familia yake, Mungu aendelee kuwa pamoja nao katika kipindi hiki kugumu cha maomboleo.
Siku iliyofuata tulisali misa maalumu ya kumuombea baba Masawe, siku hii tukiungana na ndugu zetu kutoka nyumba ya malezi Pre-Philosophy Makunganya na dada zetu masista wanaokaa katika nyumba ya malezi Mkundi. Misa iliongozwa na Padre Isaac Nabea Mbuba imc (Mlezi Pre-Philosophy) akisaidiwa na Mapadre; Wiliamu Mkalula imc, Hipolith Marandu imc, Jude Katende imc (Mlezi Pre-Philosophy). Baada ya misa takatifu tulipata muda kidogo wa kutafakali namna tulivyomfahamu na  tulivyoishi na Padre Masawe kabla ya kuondoka hapa duniani.

Pd. William Mkalula imc
Pamoja na kuonesha namna alivyomfahamu Pd. Masawe, alienda mbali zaidi akisema sifa muhimu ambazo zingetusaidia sisi kama walelewa; alimwelezea padre masawe kama mtu aliyeupenda Upadre wake na umissionari wake. Yeye alimufahamu zaidi Pd. Masawe kwasababu ya vile alivyokuwa anatimiza wajibu wake kwa umakini. Njia pekee ya kumuenzi mkuu wetu wa shirika ni kuyatekeleza na kuyafiuata yale ambayo mara zote alisisitiza hasa maisha ya jumuia na zaidi sana kuwa na nia njema na shirika na kanisa. Tujitahidi kusonga mbele daima. Yeye mwenyewe alisisitiza kwamba anamshuluru Mungu kwa sababau ni Mconsolata na anaupenda Uconsolata wake. Jitahidini kuwa wakweli na wawazi kwa walezi wenu, alisema Pd. Mkalula. Wishoni alimshuuru sana Pd. Isaac Mbuba kwa msaada wake katika maisha yake ya kimisionari kwasababu kuna wakati amewahi kufanya nae kazi huko katika parokia ya Heka.
Sr. Thelesia Ponela imc
            Sista ananza kwa kuelezea namna alivyofanya kazi na Pd. Masawe kwa miaka miwili kule Bunju kituo cha mazoezi ya kiroho akiwa kama Mkurugenzi wa Gazeti la ENENDENI hapa Tanzania. Anasema alikuwa ni Padre mchapakazi na aliyejituma katika kazi zake. Alisisitiza muda wote maisha ya familia, maisha ya kufanya kazi pamoja kwa umoja, hilo ndilo limebaki kwangu kama kumbukumbu na anaendelea kunipa changamoto katika maisha yangu ya umisionari, nijitahidi kupenda maisha ya jumuia.  Sista anaongeza kwamba anafuarahi kuwa Tanzania pamoja na matatizo yote. Matatizo yananifanya nisonge mbele kwa nguvu na bidii. Tuutafute utakatifu kwa juhudi zote, tukijifunza utakatifu wa Baba Allamano ambao haukuwa katika mambo makubwa naya ajabu bali mambo madogomadogo. Tujitahidi twende kwa pamoja na kwa ujasiri mkuu.
Pd. Mbuba  Isaac imc
            Padre alianza kwa kuuuliza swali kwamba kwanini wazuri tu? Ninapotafakari msiba huu ninakumbuka marehemu Padre Alexius Lipingu, Pd. Jachindo na waseminari wetu waliotutoka wakiwa hapa Morogoro; Frt. Nchimbi na Frt. Jackson Chengula. Tunamuomba Mungu awapokee na wawe waombezi wetu huko Mbinguni. Anatugeukia sisi sote na kutuambia “Jipeni Moyo msiogope, songa mbele, (courage). Pd. Mbuba anamshukuru Mungu kwaajili ya yote aliyofanya kwa njia ya mtumishi wake Pd.Masawe, anasema Mkuu huyu wa shirika alianza kutukumbusha wajibu wetu kama wamissionari na tusisinzie kamwe. Kwanini Mungu kamuchukua mapema hivi, wakati shirika na kanisa likihitaji sana mchango wake?
Sr. Elizabeth Msacky imc
            Nikiwa bado mdogo nilianza kujisikia wito, lakini sikuwa nafahamu chochote kuhusu mashirika haya ya kitawa na wala sikuwafahamu waconsolata. Siku moja niliona kipeperushi cha waconsolata na kwasababu Padre Masawe alikuwa anasoma pale Mwanza chuo kikuu cha Mtakatifu Augustino na mara kwa mara nilikuwa namuona anongoza misa, niliamua kumfuata kumuuliza waconsolata ni watu gani? Kwanza alinijibu kwamba yeye ni Padre mconsolata na yupo pale kwa masomo, aliniahidi kunisaidia ili niwe na wasiliano na mkurugenzi wa miito. Tangu hapo sikumfahamu mconsolata mwingine ila Padre Masawe mpaka nilipokuja kuingia nyumba ya malezi. Akawa ni msaada hata kwa familia yangu nyumbani, alimsaidia sana dada yangu katika ndoa yake. Padre Masawe kweli alikuwa mfano wa kuigwa katika maisha yake ya utume, Mungu amempenda zaidi kuliko sisi, basi tumuombee.
Sr. Suzana Kiho imc
            Padre Masawe alisisitiza sana maisha ya pamoja katika yote, nasi tujifunze kwa mfano wake. Alikuwa mtu wa kupokea watu, nasi tuwe watu kupokea wengine na kuwasaidia, na ni lazima kujiuliza mara zote katika maisha yangu watu wanaonja nini kwangu? Wanajifunza nini kwangu? Nikifa leo watu ninaowaacha waseme nini juu yangu? Watu ni lazima wajifunze Upendo wa Mungu kutoka kwetu sote, waonje faraja kwetu.
Frt. Leonard Celestine Mihafu
            Kifo kinapotokea huleta changamoto kubwa kwetu hasa kwetu sisi vijana, na kwasababu kifo huzidi hata Falsafa na Tauhidi (Teolojia) masomo tuyayasoma, basi tubaki na Imani kwa Mungu. Lakini ni lazima tujue kuwa tuna kazi kubwa ya kuwa watakatifu na kuwasaidia wengine wawe watakatifu kwa mifano yetu ya maisha ya kila siku. Lifo cha Padre Masawe kibaki fundisho kwetu na tujiulize mimi je nikifa leo itakuwaje? Wewe je ukifa leo?
Frt. Patrick (Pre-Philosophy)
            Ni wakati mgumu sana, na ni kipindi cha majozi mkubwa kwa shirika na kwa kanisa nzima la Mungu. Lakini kwa hayo tunajifunza kuvumulia magumu, tuchukue mazuri yote twende nayo na tuishi nayo ndio namna ya kumuenzi Mkuu wetu wa shirika Padre Masawe.
Pd. Hipolith Marandu imc
            Nimekuwa naye katika sehemu mbalimbali katika utume wake, nilikuwa nae Kenya wakati nikifundisha pale, baadae tulikutana Italia katika utume wake. Alisema tunataka akina Masawe wengine hapa seminarini. Tuwe watu wa maana na waungwana katika umisionari wetu, tukiwajali watu wote kama njia ya kumpeleka Yesu aliye faraja ya kweli kwa wote. Injili iwe taa ya kila mtu.